top of page
Writer's pictureOrina Ontiri

Je, unatafuta ndoto zako au mapenzi ya Mungu?

Watu husema, na hata wahubiri pia nao husema, ‘Fuata ndoto zako!’ Lakini Yesu alisema, ‘Nifuate mimi’. Ikiwa utafuata ndoto zako, unajifurahisha mwenyewe tu. Lakini ikiwa utamfuata Yesu, atampendeza yeye. Kama utafuata ndoto zako, basi unajitumikia wewe mwenyewe. Ukimfuata Yesu, utamtumikia yeye na kanisa lake. Kama utafuatisha ndoto zako, unajitengenezea njia yako mwenyewe. Kama utamfuata Yesu, yeye ndiye atakayekuandalia njia.

Kuwaambia wakristo kwamba wanapaswa ‘kufuata ndoto zao’ ama ‘kuwa na ndoto ama maono ya maisha yao yajayo’ ni kuwaongoza katika njia isiyokuwa sahihi na kuwadanganya. Hao wanaofundisha mafundisho hayo watawajibika mbele za Mungu kwa kuwadanganya waamini. Hao wanaopokea mawazo ya namna hiyo kwenye mioyo yao nao pia wanawajibika kwa kupokea kitu ambacho hakifundishwi katika biblia na ni kinyume na mafundisho ya Biblia.

Je, ni kitu gani hakiko sahihi katika wazo hili? Kwanza, hiyo siyo mafundisho ya neno la Mungu. Mambo hayo hufundishwa duniani na ‘motivational speakers’ (watu wanaowahimiza wengine wabadilishe matazamo yao na mwelekeo wao ili wafikie malengo yao na watimize uwezo wao na tamaa zao.) na waandishi na walimu wa maswala ya ‘kujisaidia’! Na wahubiri wa kikristo wameazima hayo mawazo na kujaribu kuwatia moyo wakristo kwamba wanao uwezo wa kufanya mambo makubwa, kuwa watu maalum au kubadili mambo kwenye jamii. Haya mafundisho ni ya ‘kibinadamu’ (‘humanistic) na yako kinyume na Biblia. Nimeona tovuti ya muhubiri mmoja anayejiita ‘motivational speaker‘! Inaonyesha ya kwamba siku hizi wakristo hawaoni aibu kuiga dunia na kufuatisha mifumo na mwenendo wale ili tu kuwa maarufu badala ya kuhubiri kutoka kwenye biblia. (Nitagusia katika hili hapo baadaye tena)

Pili, udanganyifu wa aina hii ya mafundisho ni kwa kwamba hayatofautishi kati ya ni vitu gani vinaweza kuwa matamanio binafsi ya Mkristo awe ama afanye kitu fulani, na mapenzi ya Mungu katika maisha yao! Badala ya waamini kuyatoa maisha yao kama dhabihu iliyo hai, takatifu, na inayokubalika mbele za Mungu, baadhi ya wakristo hasa waongofu wapya, wamekuwa wakifuata shauku zao tu katika kifanya vitu, kwa mfano, ili kuwa ‘kiongozi wa kuabudu’ ama kiongozi wa shughuli fulani ama kujaribu kumiliki studio ya kurekodia kwa sababu wanadhani wameitwa ili wawe waimbaji ama kuanzisha biashara fulani. Hawatengi muda wa kumsubiri Bwana na kutambua kama ni kweli hicho ndicho hasa Mungu anawataka wafanye! Mambo ambayo tunayataka ama kuyatamini si kwamba mara zote huwa ni mabaya, hilo liko wazi kabisa. Lakini pia ni wazi ya kwamba yale tunayoyatamani kuyafanya si mara zote ndiyo Mungu ameyachagua kwa ajili yetu! Aina hii ya mafundisho kuhusu ‘fuata ndoto yako!’ ama ‘kuwa na ndoto ya maisha yako yajayo!’ inawapendeza waamiini kwa sababu ni njia rahisi, ni njia ya mkato. Inawafanya wafikiri kwamba shauku zao binafsi za kuwa ama kufanya jambo fulani ni sawa sawa na mapenzi ya Mungu maishani mwao! Ndiyo, inawezekana wanaenda wakaomba, ‘Kama ni mapenzi yako…’, lakini kiuhalisia wanaendelea kufuata yale wayatakayo kwa sababu wanayataka sana na mafundisho haya ya kidunia yanawafanya waamini ni sawa kufanya hivyo!

Hatari mbaya zaidi ya aina hii ya mafundisho ni kwamba inawafanya waamini kufuata shauku zao wenyewe badala ya kufuata neno la Mungu, badala ya kumfuata Yesu, badala ya kufuata kile ambacho biblia inafundisha! Ni wapi ambapo Biblia inatufundisha ‘tufuate ndoto zetu wenyewe’, ama kutuhimiza tuwe na ‘maono’ kwa ajili ya maisha yetu yajayo? kama unaijua Biblia yako, utajua ya kwamba aina hii ya mafundisho hayamo popote! Watu wanatumia vibaya na kuharibu mistari ya kwenye Biblia ili kuhubiri mawazo ya kidunia na tutaangazia ni kwa jinsi gani wanafanya hivyo hapo baadaye.

Biblia inatufundisha ya kwamba chochote tunachokuwa na shauku nacho kwa ajili ya maisha yetu ya baadaye, tunatakiwa kwanza kujitoa nafsi zetu kila siku kama dhabihu iliyo hai kwa Mungu Baba, takatifu na ya kumpendeza yeye, na sio kutafuta mapenzi yetu wenyewe bali mapenzi yake (Warumi 12:1,2). Mtume Paulo anaendelea kutufundisha kwenye Warumi 12 kwamba ’haitupasi kuifuatisha dunia hii, bali tubadilishwe kwa kugeuzwa kufikiri kwetu ili tuweze kuthibitisha mapenzi mema na yanayokubalika, makamilifu ya Mungu’. Hivyo basi mafundisho ya Biblia yako wazi – jitoe nafsi yako kama dhabihu kwa Mungu na kwa kufanya hivyo acha kufikiri kwako kufanywe upya ili uweze kuelewa mapenzi makamilifu ya Mungu maishani mwako!

Neno la Mungu linatufundisha, ‘mtegemee Mungu kwa moyo wako wote; na usizitegemee akili zako mwenyewe. Katika njia zako zote mkiri yeye, nae ataelekeza njia zako’ (Mithali 3:5-6).

Hatupaswi mara zote kumtegemea Mungu afanye ama kutimiza ndoto zetu za binafsi ama maono yetu kwa ajili ya maisha yetu yajayo! Tunatakiwa kumtegemea yeye moja kwa moja ili atuongoze katika njia ambazo anataka tuziendee. Nimeona vijana wakijaribu ‘kulazimisha milango ifunguke’ ili watimize matakwa yao ama ndoto zao, na imesababisha wakose mapenzi ya Mungu kwa maisha yao, si tu kwa nje, lakini pia kwa ndani, rohoni. Kama hatutajitoa maisha yetu kwake basi mawazo yetu hayajabadilishwa na Roho wake na hatujafundishwa na Roho wake. Kwa hiyo hatutaelewa mapenzi ya Mungu, lakini pia hatutaelewa njia zake, hatutaelewa msalaba wa Yesu Kristo!

Haya mafundisho kuhusu ‘fuata ndoto zako’ hayakubadilishi kufikiri kwako kwa namna yoyote na kukufanya ujue mapenzi ya Mungu. Kinyume chake, inaruhusu shauku zetu zitutawale kwenye maisha yetu na kuelekeza maisha yetu na kutudanganya kuwaza kwamba ‘ndoto’ ama ’maono’ tuliyonayo ni sawa na mapenzi ya Mungu.

Kama nilivyosema hapo awali kwamba haya mafundisho yanaonyesha njia ‘rahisi’ kwa waamini. Ni njia ‘rahisi’ kwa sababu mwamini anaweza moja kwa moja kuchukulia hiyo shauku yake ya kuwa ama kufanya jambo fulani kwa ajili ya Mungu ndio hasa mapenzi ya Mungu kwenye maisha yake. Hakuna haja ya kuwa mvumilivu. Hakuna nidhamu ya kiroho katika maisha yake. Hakuna haja ya ‘kuthibitisha’ kama ndoto zetu ni mapenzi ya Mungu kweli. Inatufanya tuzidi kushikilia sana shauku, nia, maono na ndoto zetu wenyewe! Kama nitakuwa na mtazamo wa aina hiyo, sitaweza kuacha kukweli shauku zangu ili niweze kufanya kitu (kikubwa kwa ajili ya Mungu) katika Madhabahu ya Mungu ili Mungu aamue ni kipi kinachompendeza na kipi hakimpendezi!

Si kwamba nakuza mambo. Nimesikia wahubiri wakiwatia moyo wakristo kwamba wanahitaji kuwa na ndoto ama maono kwa ajili ya maisha. Wahubiri hawa hawawafundishi waamini kwamba wanatakiwa kutofautisha kati ya kile kinachoweza kuwa mahitaji mataka yao binafsi na mapenzi ya Mungu. Wanafundisha kana kwamba maono na ndoto ni vya Mungu! Muhubiri mmoja anaejulikana sana kule Tanzania alitumia kitabu cha Habakuki 2:4 (‘Mwenye haki wangu ataishi kwa imani…’) kuwauliza wakristo kama ‘wanayo maono binafsi kwa ajili ya maisha yao yajayo’. Mstari huu kutoka Habakuki unatimika kama kweli ya msingi katika Agano Jipya. Inarejea katika msingi mkuu wa kuhesabiwa haki kwetu na wokovu wetu! Ndio, bila shaka tunatakiwa kuishi kwa imani, lakini mstari huu hauhusiki kabisa na maswala ya kuwa na ‘ndoto kwa ajili ya maisha yetu yajayo! Msemaji alijaribu kusema kwamba kama utataka kuishi kwa imani na kumpendeza Mungu basi unatakiwa kuwa na ‘ndoto kwa ajili ya maisha yako ya baadaye’. Hii haina maana na ni upotoshaji mkubwa wa maneno ya Mungu. Mambo haya hufundishwa duniani na waandishi na wasemaji ambao hawamjui Mungu wala wokovu wake, lakini wanataka kuwaonyesha watu ni namna gani wanaweza kufanikiwa katika maisha yao na kuwatia moyo kwamba wanayo ‘hazina’ (potential) au ‘uwezo’ ya kufanya mambo makubwa sana na maisha yao. Bila shaka watu hupenda kusikia mambo mazuri kuwahusu wao na kuambiwa kuwa wanaweza kufanikiwa na kupata vitu. Inavunja moyo sana kuona wasemaji na waandishi wa kikristo wanaacha neno la Mungu na kufundisha filosofia na saikolojia ya dunia hii ili kuwavutia wasikilizaji.

Yesu alisema kwamba chakula chake ni kutenda mapenzi ya Baba yake. Akasema kwamba, hakuja kutenda mapenzi yake binafsi bali mapenzi ya Baba aliyemtuma na alitafuta kutofanya mapenzi yake bali ya Baba, na kwamba wakati wote alifanya mambo ya kumpendeza Baba. Kama mwana wa Mungu aliishi hivi, kwa nini sisi tusiishi? Ni kwa nini wahubiri wa leo wasifundishe Biblia badala ya mawazo ya kibinadamu? ‘Fuata ndoto zako’ ndicho kitu ambacho dunia inawaambia wale watu wasiomjua Mungu.

Muhubiri mwingine maarufu sana Tanzania, ambaye pia anachukuliwa kama Nabii, alifundisha mawazo kama yafuatayo:

Imani huja kwa kusikia. Mwanzo wa imani ni kusikia. Sikiliza vitu vile tu ambavyo vitakuwa ni vizuri kwa ajili ya maisha yako yajayo. Kuwa na shauku ya kusikiliza vitu vile ambavyo vitasababisha maisha yako yajayo yawe mazuri. Unataka kwenda wapi? Unataka kupata kitu gani? Andaa / chagua malengo yako ya kufanikisha. Andaa mkakati amabo utakufikisha pale. Tumia muda mwingi katika kufikiri kuhusu vitu ambavyo vitakuletea faida, chukua kalamu na karatasi, andika malengo yako. Kila mafanikio yana gharama zake, lipa gharama za mafanikio.

Mtume Paulo anaongelea kuhusu hao wanaoliharibu neno la Mungu (2 Wakor 2:17), na hicho ndicho hasa muhubiri huyo hapo juu anachokifanya. Anachukua mstari unaofahamika vizuri lakini haunukuu mpaka mwisho. Imani haiji tu kwa kusikia! Unaweza kusikia mambo mengi tofauti tofauti, mengi katika hayo yakakupoteza! Imani huja kwa kulisikia neno la Mungu! Lakini huyu muhubiri hakuisema kweli hii! Badala ya kuhimiza watu waliamini neno la Mungu, anafundisha mawazo ya kibinadamu, ni mawazo ya dunia hii! Anahimiza hamu zao binafsi na kiburi. Anawahimiza wafikiri kuhusiana na nafsi zao wenyewe, ni kitu gani wao wenyewe wanataka kukipata, nini kitawanufaisha, na anawafundisha kutumia muda wao mwingi kwa ajili ya mikakati itakayowasaidia kufikia malengo yao! Haya ni mawazo ambayo yamekuwa yakifundishwa duniani leo na viongozi wa kikristo wamekuwa wakiweka mawazo haya kwenye mitandao kama Facebook kana kwamba yalitokea kwenye Biblia, na wakristo wengi wamekuwa wakiyasoma na kuyapenda! Inaonyesha wengi wanalipuuza neno la Mungu. Inaonyesha tunapenda kuambiwa ni jinsi gani tunaweza kuwa wenye mafanikio, ‘hazina’ (potential) zipi tunazo, tu wazuri kiasi gani, ni mitazamo ipi ya kufanya ili tuwe wenye mafanikio na kukubalika kwa watu wengine. Ni kwa nini hii haikuwa sawa? Kwa sababu inatuhimiza kuzipenda nafsi zetu badala ya kumpenda Mungu na kujikana wenyewe.

Biblia inatufundisha kwamba ‘mwisho’ hautakuja mpaka utakapokuja ule ‘upotofu mkubwa’ wa kuiacha imani. (1Tim.4:1,2; 2 Thes 2:3). Hivyo, moja kati ya ‘alama’ za nyakati za mwisho, idadi kubwa ya waamini wataikana imani. Je tunachokiona ni mwanzo wa hatua hizo? Duniani kote, wahubiri mashuhuri na wasemaji wanawajaza wakristo wadogo na mawazo haya na filosofia ya dunia, na wakristo wadogo wengi wanayajenga maisha yao katika ‘mchanga’ huo badala ya ‘mwamba’. Ni inawezekana kabisa kwamba wengi wa hawa wakristo wadogo wataanguka katika nyakati za majaribu kwa sababu wamekuwa wakijenga mchangani.

Unajua Biblia inachokifundisha, msomaji wa kikristo! Neno la Mungu linatufundisha, ‘Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na hayo mengine yote mtazidishiwa’. (Matt 6:33). Je, ni kwa nini hawa wahubiri wa kisasa wanapuuza kweli hii rahisi, ya msingi na yenye nguvu? Na Bwana alisemaje, kumwambia Baruku ambaye alikuwa msaidizi wa Yeremia? Mungu alisema, ‘na unajitafutia vitu vikuu kwa ajili yako mwenyewe? Usivitatufe…’ Bila shaka mstari huu una mazingira yake hasa, lakini ni neno ambalo Mungu anaweza kulifanya katika mioyo yetu, (kama alivyofanya kwangu), hasa pale tunapokuwa tumechukuliwa na ndoto na mawazo yetu! Tayari nimeshanukuu mstari wa kwanza na wa pili wa Warumi 12 kuhusu kujitoa maisha yetu kama dhabihu iliyo hai, na kuthibitisha ni lipi ama ni yapi mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu. Sikiliza mstari unaofuata unavyosema, ‘Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kuliko ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani (Warumi 12:3). Unaona, Paulo anajua ya kwamba tunaweza kuchukuliwa na mawazo makubwa kwa ajili ya nafsi zetu na maisha yetu na akatuonya kuhusu majaribu hayo! Wahubiri wa sasa wanahamasisha waamini wasitambue hili jaribu bali wafanywe mateka ya jaribu hili!

Yesu alipokuwa akiongelea kifo chake cha msalabani, Petro alimzuia. Petro hakupenda lile wazo la ‘udhaifu’ na ‘kushindwa’. Petro alikuwa na ‘maono’ tofauti kwa ajili ya huduma ya Bwana wake Yesu Kristo. Yesu alimgeukia na kumwambia, ‘Rudi nyuma yangu, shetani, wewe ni kikwazo kwangu: maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya kibinadamu (Matt 16:23). Na hivyo leo, wahubiri na wasikilizaji wote kwa pamoja wanapenda vitu vinavyoongelea uthabiti na mafanikio ya ‘hazina’ (potential) au ‘uwezo’ za watu, ya kufikia ‘malengo’ ya kutimiza ‘ndoto’ yako na kuwa na ‘maono’! Haya mambo si ya Mungu, bali ya wanadamu. Katika mstari unaofuatia Yesu anasema, ‘kama mtu yoyote anataka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake na anifuate.’

Katika mstari hapo juu Petro alimkemea mwana wa Mungu. Petro alikuwa na mawazo yake ni kwa jinsi gani Yesu angeweza kuubadili ulimwengu. ‘Maono’ yake kwa Yesu yalielekea sana kwenye fikra za kibinadamu za nguvu, ushindi na mafanikio. Yesu si kwamba tu alidhihirisha kwamba fikra za Petro zilikuwaza ‘kibinadamu’ lakini pia zilikuwa zimehamasishwa na shetani.

‘Mpango’ wa Petro kwa ajili ya huduma ya Yesu ulionyesha kiburi cha kibinadamu, ambaye alitaka kuwa na mafanikio na maarufu – ni kiburi na kuamini katika uwezo wake binafsi, ambacho bila shaka hutoka kwa shetani. Wahubiri na mashirika leo hii kwa namna moja yanarudia kosa la Petro. Wanawaambia vijana pale Tanzania kwamba kama wakiwa na mtazamo sahihi, wakiwa na namna sahihi ya kufikiri wanaweza kuibadilisha nchi – kwa kiasi ni kama vile tu Petro alivyokuwa anajaribu kumwambia mwana wa Mungu ni jinsi gani angeweza kushinda kwa ajili ya Israeli! Na wao wanakosea kama vile Petro! Na wanadanganyika kama Petro kabla Yesu hajamkemea kwa kiburi chake! Badala ya kumuhubiri Kristo na kusulubiwa kwake, na kuwafanya wasikilizaji wao wawe wafuasi wa kweli wa Kristo amabo wanaweza kuishi na kuisambaza Injili, wanachokifanya ni kuwahamasisha vijana kuamini zaidi kwenye uwezo wao binafsi ili kuubadili ulimwengu – wanachohitaji ni mtazamo sahihi tu.

Unaweza kuona kwenye Facebook. Wakristo wanaweka mawazo ya kibinadamu tu, si ya kibiblia, kuwaambia wengine kwamba maisha yao yanaweza kuwa mazuri, ya furaha na mafanikio zaidi kama watakuwa na mtazamo sahihi. Saa zingine hawajerei kwenye Biblia kabisa, ni mafindisho tu ya filosofia ya kisasa ya mwanadamu! Hayatokani na Biblia, lakini wakristo ‘wanapenda’ mawazo hayo na wanatiwa moyo nayo!

Petro alitaka kuubadili mtazamo wa Yesu, Mwana wa Mungu kuhusiana na mapenzi ya Mungu kwake! Lakini Yesu alitembea katika ushirika na Baba yake na alitafuta tu mapenzi ya Baba yake, sio Yake mwenyewe. Alitaka tu kuyafanya yale yaliyompendeza Baba – hata kama ingeonyesha kutokuwa na umaarufu, ‘kutofanikiwa’ na kufa kwa udhaifu msalabani! Wako wapi wanaoihubiri kweli kama ilivyo katika Yesu? Wako wapi wanaouhubiri kweli kama ilivyofundishwa na Yesu? Wako wapi wanaoyafundisha maisha ambayo Yesu aliishi?

Tafadhali usinielewe vibaya, bila shaka vile tunavyowaza ni muhimu, muhimu sana. Lakini Biblia haitufundishi hivyo kwa kusema, ‘mtazamo sahihi’ tunaweza ‘kufanikiwa’ katika kubadili mambo. Inamfundisha Yesu, inafundisha hivi,

“Iweni na nia iyo hiy ndani yenu ambayo ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa mwanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama la mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtiihata mauti, naam, mauti ya msalaba. (Wafilipi.2:5-8)

Wahubiri wa leo wanafuata dunia na mafundisho ya ‘kujithibitisha mwenyewe’ au ‘self-realisation’ (jinsi gani ya kutimiza ndoto zako na maono na jinsi ya kufikia malengo yako) na sio ‘kujikana’.Wanafundisha saikolojia ya kibinadamu na wanajaribu kuivisha vazi la kibiblia! Kama unataka kuwa na ‘lengo’ katika maisha yako, kuwa na hili hapa…

‘Nawe mpende BWANA Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote’ (Kumb, 6:5).

Fanya hivi, nawe utabarikiwa kupita kipimo. Fanya hivi, na yeye atakuongoza katika njia anazozitaka uziendee. Fanya hivi, kwa sababu anastahili. Amekuokoa na kukusafisha ili usiishi tena kwa ajili yako mwenyewe, bali kwa ajili yake ambaye alikufa kwa ajili yako (2 Wakor 5:15). Fanya hivi, kwa sababu wewe si mali yako bali umenunuliwa kwa thamani (1 Wakor 6:20,21). Fanya hivi, kwa sababu yeye ni Mungu!

Huna haki na ndoto zako mwenyewe, kwa maono yako mwenyewe, kuyafikia malengo yako binafsi, kutimiza uwezo wako na tamaa zako (1 Wakor.6:19,20). Tumesulubiwa pamoja na Kristo! Haki yetu yote kwa nafsi zetu zimesulubiwa pamoja naye! Sisi ni mali yake! Utukufu umrudie yeye! Atatuchagulia njia ambayo tutakwenda. Atatufanya tuwe watu ambao tunamtumikia BWANA katika kweli, haijalishi kazi tunayofanya; atatufanya tuwe ni watu tunaolitumikia kanisa lake, na sio kutumikia nafsi zetu. Ndipo tutakapomtumikia siyo kadiri ya uwezo wetu bali kwa neema Yake! Mtume Paulo anatufunnulia ni muhimu kiasi gani hili jambo lilivyo na ni kwa jinsi gani inatishakama tutashindwa kutofautisha kati ya shauku zetu wenyewe na mapenzi ya Mungu.

‘Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakaeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu.’ (Wafil 2:20-21).

Cha kushangaza, Paulo anatuambia hapa kwamba kati ya hao wote wanaosema wanamtumikia BWANA, hana mtu ambaye anaeweza kumfananisha na Timotheo, ambaye anawajali kwa dhati watu wa Mungu na ambao wanamtumikia Mungu kwa dhati! Katika muda huu kwenye huduma yake, Paulo anasema kwamba watu wengine wote wanajitumikia wao wenyewe tu! Wanajitafutia faida zao wao wenyewe tu; wanatafuta kufikia malengo yao tu na kutimiza shauku na ndoto zao za mafanikio, kujulikana, uwezo na pesa. Hili ni neno kubwa sana. Kama ingekuwa hivi wakati wa siku za Paulo, ingeweza kuwa kweli leo, na mzigo wangu ni kwamba hawa wahubiri wanaofundisha ‘maendeleo binafsi’ na ‘kujitosheleza binafsi’ kwa kuwapa moyo waamini kufuata ndoto zao na kuwa na maono kwa ajili ya maisha yao yajayo, wanawaelekeza waamini wawe kama wale waliokuwa wanasemwa na Paulo kwamba ‘wanajitafutia wenyewe tu’ na sio kwa ajili ya Kristo. Nimeshakutana na vijana wanaosema wanataka kumtumikia Mungu katika huduma ama waimbaji. Niliona kinachowaendesha ni tamaa zao na hamu zao kufanya kile kinachowapendeza. Na nimewaona wakifuatisha ndoto zao na mwisho wake wanakosa chochote kwa kuendeshwa na tamaa zao. Kwa upande mwingine, wapo wale wanaomtafuta Kristo kwa ajili yake na sio kwa faida zao binafsi; wanautafuta kwanza ufalme wa Mungu; hawajitafutii njia yao wenyewe bali wanayatoa maisha yao kwa Mungu; hawatafuti kujiridhisha nafsi zao – basi wanaishi kwa kujikana nafsi zao na kumpenda Kristo Yesu. Watu kama hao ndio Mungu huwaita na kuwatumia!

Tafadhali naomba unielewe. Ni vizuri kutamani kumtumikia Mungu! Lakini tatizo ni hili: siku hizi wahubiri wengi wanaweka msingi mwingine, na siyo Yesu Kristo! Badala ya kufundisha Yesu na Neno la Mungu, wanafundisha mawazo ya kibinadamu, ya saikolojia ya dunia hii. Ndiyo, wanatumia mistari ya Biblia, lakini kama tulivyoona, wanaitumia mistari ile kujenga mafundisho yao yasiyo na msingi wa kweli. Wanachochea vijana wafanye mambo mengi au kazi kubwa, lakini wanaongoza vijana kujenga juu ya msingi wa miti, majani na manyasi, na msingi huo hauwezi kuleta ufalme wa Mungu! Na Paulo anasema kama tukijenga juu ya msingi mwingine kazi yetu itateketea nasi tutapata hasara. (1 Wakor.3:10-15). Ni kwa ajili hayo ninaiandika makala hii fupi. Ni hamu yangu tumtumikie Mungu kaitka mambo yote, na umjue Yeye na mapenzi Yake na usipate hasara siku ile!

Tuko katika mikono ya Baba yetu. Tunatakiwa kukabidhi njia zetu kwake kwa ukamilifu. Katika Zaburi 37:3,4 inasema,

‘Umtumaini BWANA ukatende mema, ukae katika nchi upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa BWANA, naye atakupa haja za moyo wako’.

Hii ni kweli ya kushangaza sana. Kama tutamfanya Bwana kuwa ndiye furaha yetu; kama tutamtafuta yeye kuliko kitu chochote katika hii dunia; kama tutampenda yeye kuliko kitu chochote duniani; kama tutaishi kwa kupenda kutii neno lake; kama tutamtumaini atuongoze, basi mioyo yetu na akili zetu zitafanywa kwa upya na Roho wake, tutajikuta tuko katika mapenzi yake naye atatupa mahitaji ya mioyo yetu. Kama tutataka kitu ambacho kiko kwenye mapenzi yake, basi mioyo yetu itakuwa imeandaliwa na kuwa na furaha kutoa dhabihu hii kwa Bwana na kumsubiria yeye atupe njia kwa ajili ya maisha yetu!

Vitabu vingi vimeandikwa na watu wasiokuwa wakristo zaidi ya miaka 50 iliyopita kuhusiana na ‘maendeleo binafsi’, jinsi ya kuwa mwenye mafanikio, kufikia malengo yako, kuwa na mtazamo sahihi, kufikia uwezo wako, kuwa na maono kwa ajili ya maisha yako yajayo na kufuata ndoto zako. Kinachotokea ni kwamba wahubiri wa kikristo na waandishi wanaazima moja kwa moja toka kwenye hizo filosofia, na mipangilio hiyo ya kisaikolojia, kwa kutumia maneno yale yale, na kuyatoa kama ni mafundisho ya kibiblia! Hayo sio mafundisho ya kibiblia. Hayana uhusiano wowote na msalaba wa Yesu Kristo. Inahusika na kuipamba ajenda yangu, na sio ya Bwana. Tunatakiwa kujali sana onyo la Paulo katika Wakol.2:8, ambapo anasema, ’Angalieni mtu asiwafanye mateka, kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo’. Paulo anasema kwamba ni lazima ‘ukitumia halali neno la kweli’ (2 Tim2:15) lakini wapo wengi ambao ‘wanapotosha neno la Mungu’ (2 kor2:17). Ni kwa jinsi gani watu ‘wanapotosha’ neno la Mungu hivi leo? Wanafanya hivyo kwa kurejea kwenye mistari ya kwenye biblia na kuitumia vibaya mistari hiyo kujenga mafundisho yao binafsi. Wanafanyaje hivyo kuhusiana na ‘ndoto’ na ‘maono’? Wanafanya hivyo kwa kurejea kwa habari ya Yusufu katika Agano la Kale.

Wanasema kwamba Yusufu alikuwa na ndoto na kwamba ndoto hizo zingeweza kumuongoza awe mwenye mafanikio katika maisha yake ya mbeleni. Kwa hiyo wahubiri hawa wanawatia moyo waamini wawe na ndoto, kwa sababu kwa kupitia kuwa na ‘ndoto’ ama ‘maono’ kwa ajili ya maisha yako ya mbeleni ya kwamba utaweza kuyafikia malengo yako! Hii yote haina maana na ni udanganyifu mtupu. Na wanasema pia kwamba unatakiwa uwe mwangalifu jinsi unavyofanya na ndoto zako – na ni nani unamshirikisha ndoto zako. Kama utamshirikisha mtu ambaye si sahihi basi unaweza kuingia kwenye matatizo makubwa sana na inawezekana ndoto yako isitimie. Hii haina maana na ni udanganyifu!

Muhubiri mkubwa Africa alifundisha mawazo haya:

Kama hautakuwa na ndoto umeridhika kubaki kutokuwa na kitu. Kama hautakuwa na maono ya kuwa na viatu viwili, kiatu kimoja kitakufurahisha. Nakuomba hii leo uwe na ndoto. Kama hautakuwa na ndoto, hauna kitu cha kupambana kwa ajili yako. Kama hautakuwa na ndoto, wewe utakuwa umeridhika. Ota ndoto kwa ajili ya familia yako, kanisa, mji….. tambua ni mtu gani wa muhimu maishani mwako – mtu sahihi anaeweza kuyanyanyua maisha yako na kunyanyua hali yako. Na macho yako yafunguliwe sasa ujue ni watu gani wa kukunyanyua na kuinua hali yako. Ota! Kama una ndoto za kumiliki gari, utatafuta rafiki ambaye anamiliki gari…. Ota!

Wakati akiongea hayo, mamia ya waamini katika muhadhara wake pale Tanzania walisimama na kupiga kelele na kupunga mikono yao hewani. Wakadhani kuwa huu ni ujumbe wa kushangaza sana – wakadhani ni neno la Mungu, kwa sababu muhubiri alikuwa akitumia mfano wa Yusufu toka kwenye biblia. Kitu alichokuwa anakifanya ni kulipotosha neno la Mungu. Yote hapo juu ni mambo yasiyo na maana na ni udanganyifu – tatizo ni kwamba wakristo wengi wanapokea udanganyifu huo badala ya kuthibitisha vitu hivi kwenye Biblia!

Acha nikushirikishe kitu fulani rahisi ambacho kilinisaidia mimi kwa kiwango kikubwa kwa miaka mingi. Kama mtu yoyote akifundisha kitu kipya ama tofauti ama hukitambui toka kwenye Biblia, jiulize, ‘Hii imeandikwa wapi kwenye Biblia?’ Kwa mfano, muhubiri hapo juu anawaambia wasikilizaji, ’Kama huna ndoto, huna chochote cha kupigania.’ Haya ni mawazo yaliyo madogo kwa uwazi. Kama ni kweli, ni muhimu kwetu kuelewa hili. Kwa hiyo ni wapi nitayapata kwenye Biblia, zaidi hasa, haya yanapatikana wapi kwenye Agano Jipya?

Jibu haliko popote! Hakuna kitu kama hiki kinachofundishwa na Biblia. Ni ubunifu tu wa msemaji. Madanganyo haya yanawafundisha waamini kutilia mkazo kwenye nafsi zao wenyewe, kuangalia zaidi kwenye maendeleo yao binafsi na faida – inaangalia zaidi ‘kwangu’ na sio kwa ‘Yesu’! Hivyo inahamasisha kiburi kwa waamini (‘tambua nani ni wa muhimu maishani mwako’. Yesu hakufundisha hivi!). na pia inahamasisha uchoyo. Muhubiri hapo juu anasema ya kuwa kama huna ndoto ya viatu viwili utaridhika na kiatu kimoja. Hii si kweli! Mtu mwenye kiatu kimoja anajua ya kuwa anahitaji kiatu kingine. Biblia haifundishi ,’ota ndoto za nguo, ama vyakula.’ Yesu anatufundisha ‘kutafuta kwanza ufalme wa Mungu’ kwa sababu Baba tayari anajua ya kuwa tunahitaji vitu hivyo! Huyu muhubiri anaendelea mbele na kusema kwamba kama huna ndoto za gari, utaishia kuwa na baiskeli, lakini kama una ndoto za gari, utakutana na mtu mwenye gari – na baada ya hapo ndipo ndoto yako itatimia! Hii inachochea uchoyo ndani ya waamini. Anasema kwamba unatakiwa kuwa na ndoto za kumiliki gari kama unataka kuwa na gari! Haya ni madanganyo na ni ukatili! Nimeongea katika vijiji vingi Tanzania na ninafahamu ni jinsi gani watu maskini wako, na mtu huyu anadanganya watu kwa kudai kwamba njia ya kupata gari ni kwa kuwa na ndoto ya kuwa na gari! Anachochea hamu ya ‘vitu’ tu ndani ya watu, na sio pendo kwa Mungu. Biblia inatufundisha ‘kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu’! Biblia haifundishi, kama unataka kitu, unahitaji kuwa na maono yake!

Kama nilivyosema pale mwanzo, mafundisho haya hayatofautishi kati ya shauku zetu binafsi (‘ndoto’) kwa ajili ya maisha yetu yajayo na mapenzi ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu. Na hiki ndicho hasa muhubiri hapo juu alichofanya! Anatumia kilichotokea kwa Yusufu kwenye haja na matamanio binafsi! Ngoja tuangalie ni kwa jinsi gani neno la Mungu linavyopotoshwa na watu hao.

Kitu cha kwanza na muhimu, ndoto mbili ambazo Yusufu aliota zilikuwa zimetoka kwa Mungu moja kwa moja. Hakukaa chini ya mti na kuwaza ni kwa jinsi gani atakuwa mtu mwenye mafanikio siku moja! Hakujitengenezea ndoto binafsi ya kuwa mtu mkubwa! Hakusema, ‘nataka nimtumikie Mungu kwa namna hii ama namna ile na siku moja nitafanya yote ninayoweza ili nifikie lengo langu kwenye maisha’! Ndoto zake zote mbili zilikuwa ndoto za kweli. Hazikuusika na nafsi ya Yusufu. Alipewa toka kwa Mungu. Hazikuwa zinahusika na maono binafsi ya Yusufu kwa ajili ya maisha yake. Mungu mwenyewe alikuwa anawasilisha kile ambacho Yeye Mwenyewe alikuwa anataka kufanya kupitia Yusufu. Ndoto hizi zilikuwa ni mapenzi ya Mungu kwa Yusufu – chochote kile ambacho Yusufu alikitaka ama kutokitaka kwenye maisha yake, haya yalikuwa ni mapenzi ya Mungu! Ndoto hizi ziliwakilisha mapenzi ya Mungu toka mbinguni, si kwa Yusufu tu, lakini pia ilihusu mapenzi ya Mungu kwa maisha ya baadaye ya taifa la Israeli! Zaidi ya hayo, maisha ya Yusufu na jinsi Mungu alivyomuongoza ilikuwa na maongozi kwa wakristo wote kwa karne nyingi. Ni kwa jinsi gani wahubiri wa sasa wakaliharibu neno la Mungu kwa kufananisha ndoto aliyoota Yusufu ambayo ilitoka kwa Mungu moja kwa moja na ambayo chimbuko lake haikuanzia kwenye hamu na matamanio ya Yusufu mwenyewe, kwa lengo la mtu la kutaka kuwa mtu fulani au kuwa na mafanikio katika biashara? Ni kwa jinsi gani huyo muhubiri anafananisha ndoto aliyoota Yusufu ambayo alipewa na Mungu na ‘ndoto’ mtu aliyonayo ya kuwa na gari? Na ni kwa namna gani wakristo wengi wanaweza kudanganyika kirahisi na mafundisho hayo ya uongo? Je, ni kwa sababu kupenda kwetu mafanikio kwenye huduma ama biashara kumekua kukubwa kuliko kumpenda Mungu? Ndiyo maana tunaweka utulivu mkubwa kwa waongo hawa kuliko neno la Mungu kwa sababu tu wanatuahidi vitu vikubwa!

Mafundisho haya si sahihi hata kidogo katika kila eneo. Tumeambiwa, “Kuwa makini ni mtu gani unayemshirikisha ‘ndoto’ zako. Angalie kile kilichotokea kwa Yusufu pale aliposema kuhusiana na ndoto zake! Kama utawaambia watu ambao si sahihi kuhusiana na ’ndoto’ yako, wanaweza kukucheka na kuifanya ‘ndoto’ hiyo kutotimia.” Mafundisho haya huamsha hofu na ni ushirikina. Kwa sababu wahubiri hawa hawatofautishi kati ya matakwa binafsi na mapenzi ya Mungu, sasa wameamua kubuni mafundisho ya ‘kulinda’ hizi ndoto binafsi kwa kusema, ’usimwambie kila mtu ndoto zako!’

Ngoja tuwe wawazi. Kile Mungu alimuonyesha Yusufu kilikuwa ni mapenzi yake. Hakuna mwanadamu wala shetani ambaye angeweza kuzuia kutimia kwake! Wote kwa pamoja, watu na shetani walijaribu kuzuia, lakini ilishindikana kwa sababu Mungu mwenyewe alilisema hilo! Kile Mungu aliahidi, alitimiza. Yusufu aliwaambia kaka zake kuhusiana na ndoto zake na akaingia kwenye matatizo. Biblia haisemi kama Yusufu alikosea kwa kuwaambia kaka zake kuhusiana na ile ndoto. Lakini kilicho wazi ni kwamba Mungu alitumia kupinga kwao (kwa kumtupa kwenye shimo na baadaye kumuuza Misri) kulitimiza azimio lake! Bwana apewe sifa! Mungu alitumia maamuzi ya kikatili ya kaka zake na Yusufu kulitimiza kusudi lake. Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani hawa wahubiri wa leo wanariharibu neno la Mungu.

Bila shaka, Yusufu hakujua mwanzoni ni kitu gani Mungu atakwenda kufanya na yeye. Yusufu angehitaji kuthibitisha. Angehitaji kuwa na tumaini kubwa sana kwa Mungu; angeweza kuhitaji ajifunze kutoka kwa Mungu; angehitaji uvumilivu zaidi! Lakini ahadi ya Mungu ilikuwa kweli! Tafadhali lielewe hili. Yusufu hakuwa na ‘ndoto’ ya kuwa kiongozi wa Misri! Yeye mwenyewe hakuwa na hitaji binafsi la kuiongoza Misri na kumsubiri Mungu aikamilishe ‘ndoto’ yake. Alipata ndoto mbili za wazazi na kaka zake wakimuinamia, na hakujua ilikuwa inamaanisha nini! Hakujua nini mapenzi ya Mungu yalikuwa hasa kwenye maisha yake! Mapenzi ya Mungu kwenye maisha yake yalikuwa yakiendelea hatua kwa hatua kwa miaka mingi hata bila yeye kutambua kwa wakati mmoja. Kwa muda wa miaka mingi, Mungu alitaka tu Yusufu amtumainie, ampende na kumtii. Kwa wakati muafaka Mungu angeweza kuweka mipango ama mapenzi yake wazi na anageweza kuwa ndiye wa kuzikamilisha! Na hivyo ndivyo Mungu anavyofanya kazi katika maisha yetu.

Anatutegemea sisi tutembee kwa utii mbele zake; kumpenda kwa akili, mioyo na nafsi na nguvu zetu zote; kujikana wenyewe sio kutafuta mapenzi yetu wenyewe bali mapenzi yake. Kama tutaishi hivi mbele zake, hatutakuwa na haja ya kubeba baadhi ya ‘maono’, hatutakuwa na haja ya kukimbizana na baadhi ya ‘ndoto’, kuhofia kuwa kuna mtu anaweza kuzuia kutokea kwake kama tutaongea kwa wakati usio sahihi! Kuishi kwa namna hii, tutakuwa tumebarikiwa kikweli, na baraka yetu kubwa, zawadi yetu kubwa ni Bwana mwenyewe! Kuishi namna hii, kutakuwa ni kubadilishwa kwa mioyo ya akili zetu na tutakuwa na uwezo wa kutambua nini ni mapenzi ya Mungu kwetu na yapi sio. Bwana mwenyewe ataweka shauku sahihi katika mioyo yetu, ama kuthibitisha kwamba ile shauku iliyoko katika mioyo yetu imetoka kwake. Kwa ujumla, Mungu hufunua mapenzi yake hatua kwa hatua. Hakuna njia ya mkato. Mungu atapima mwamko wa mioyo yetu; tutahitaji utii, uvumilivu na imani. Kama tutatembea hivi mbele zake, hakuna chochote wala mtu yeyote ambaye ataweza kuzuia mapenzi yake yasitimie kwenye maisha yetu. Mioyo na akili zetu zitakuwa na amani; hatutachanganyikiwa kusubiri ‘ndoto’ na ‘maono’ yetu kutimia.

Kama tutatembea kwa unyenyekevu mbele zake, kujitoa nafsi zetu kwake, basi atatuonyesha wakati wowote kama tunakosea katika kile ambacho tunakitaka ama kukitamani. Atatuonyesha kwa kupitia neno lake ama kupitia matukio, na kwa kutupa amani ndani ya mioyo yetu kuhusiana na lile ambalo liko sawa. Tafadhali naomba usinielewe vibaya. Sisemi kwamba watu kama Yusufu pekee ndio wanaoweza kujua wito wa Mungu katika maisha yao, hapana, hapana kabisa. Sisi twaweza pia. Lakini tatizo na udanganyifu ni kwamba watu wanasema vitu ninavyovitaka ama kuviota ndivyo hivyo hivyo mapenzi ya Mungu!

Mungu alimuahidi Abrahamu mtoto. Abrahamu alisubiri kwa muda mrefu sana ili ahadi hiyo iweze kutimia. Alikuwa bado akisubiri hata pale Mungu alipomtokea kwenye Mwanzo 15 na kusema,

‘Usiogope Abrahamu: mimi ni ngao yako, na ni thawabu yako.’

Abrahamu alikuwa na hofu kwamba bado hakuwa na mtoto, lakini Mungu alimwambia, ‘Mimi ndiye thawabu yako.’ Je hii ni kweli kwangu mimi na wewe, mpendwa msomaji? Unamuhesabu Yesu Kristo kama thawabu yako kubwa, kuliko kitu kingine chochote? Je, Yeye ni wa thamani kwako kuliko hata karama zako au mwito wako? Je, Yeye ni thawabu kubwa kwako kuliko ‘ndoto’ na ‘matamanio’ yako? Kama sivyo, anawezaje kukutumia?

Mungu alimpa Abrahamu mtoto, jina lake Isaka. Mungu alitimiza ahadi yake kwa wakati wake na kwa njia zake. Wakati Isaka bado akiwa mdogo, Mungu akamwambia Abrahamu amtoe sadaka ya kuteketezwa. Abrahamu hakusita. Asubuhi na mapema Abrahamu aliamka kumchukua mtoto kwenye eneo la kutolea sadaka – eneo ambalo hapo baadaye Yesu Kristo alikuja kusulubiwa. Tunahitaji kuelewa ni jinsi gani ile dhabihu ilikuwa kubwa kwa Abrahamu. Si tu Isaka mwanae wa pekee, aliyepewa kimuujiza na Mungu lakini Mungu aliahidi kutengeneza taifa kupitia kwa Abrahamu na kwamba uzao wake utakuwa kama nyota za angani! Mungu alimuahidi Abrahamu kwamba jamaa zote za dunia zitabarikiwa kupitia yeye na uzao wake! Kwa hiyo ahadi za Mungu kwa baraka zijazo ambazo zingekuja kukamilishwa kupitia Isaka, na Abrahamu si kwamba tu alimtoa mwanae wa pekee, ambaye alimpenda, lakini pia kumtoa kama dhabihu ya ahadi zote ambazo Mungu alimuahidia, kama Isaka angekufa, mahadi ya mungu pia ingekuwa imechinjwa!

Inakuwaje kwako? Uko tayari kuweka kando mipango yako binafsi, matamanio ama ndoto kwa hili ama kwa lile ’kwenye madhabahu’ na kusema, si mapenzi yangu bali ya kwake ndiyo yafanyike! Je uko tayari ‘kuachilia’ yale unayotaka kufanya, ama yale unayoyawaza kwamba Mungu amekupangia, na umuache yeye ‘afufue’ kile alichokichagua kwa ajili yako? Abrahamu, alipokwenda kumtoa Isaka, aliwaambia wajakazi wake wasubiri wakati yeye anaenda ‘kuabudu’. Je, unaweza kumuabudu Mungu kwa njia hii – kumfanya yeye ngao yako na thawabu yako kuu, kumpenda yeye kuliko huduma yoyote ama mafanikio ambayo umekuwa ukiyaota? Je, mambo mengine yanaonekana kama si kitu kwako ukilinganisha na kumjua yeye na kumpenda yeye na kutembea katika njia zake? Kama sivyo, atawezaje kukutumia? Kama sivyo, Mungu atawezaje kuwabariki wengine kupitia wewe? Kama ‘tutamwabudu’ Mungu kwa jinsi hii, hatutapoteza! Mungu mwenyewe atatupa kile tunachotaka na kutupa njia tutembee na kubariki wengine kama sisi wenyewe!

WAZO LA MWISHO:

Mapenzi ya Mungu kwa maisha yangu ni nini? Paulo anasema, “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu…” (1 Wathes.4:3) Anaendelea kufundisha kwamba, “Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.” (1 Wathes.5:18) Je, naweza kujua mwito wa Mungu kwa maisha yangu?

Ndiyo, naweza! Paulo anatusihi, “mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo;” (Waefeso 4:1,2)! Zaidi ya hayo Paulo anatujulisha kwamba, “Mungu…alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake.” (2 Tim.1:9). Na Petro anathibitisha ukweli huo, “…kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote…” (1 Petro 1:15). Katika Waebrania tunaambiwa jambo la ajabu juu ya mwito wetu, “Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana…Yesu.” (3:1). Hii ni neema kubwa sana kwetu; tumeitwa na mwito wa mbinguni; tuwe kama Yesu Kristo ulimwenguni humu! Sawasawa na mafundisho ya Yohana, “…kama Yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu.” (1 Yoh.4:17). Na Paulo anaeleza ukweli mkuu sana, “Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea; katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima.” (2 Wakor.2:15,16). Huo ndio mwito mkuu, siyo ndiyo? Je, tunautafuta mwito kuu kuliko huo? Kama ni hivyo, labda Mungu ataongea nasi kama vile alivyoongea na Baruku aliposema, “Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute!” (Jer.45:5). Sisi tumeitwa tuwe harufu ya Kristo mbele za Mungu kwanza na kwa kimsingi. Tunaishi mbele ya Mungu kwanza, siyo mbele ya watu. Bila kuwa harufu ya Kristo mbele ya Mungu, hatuwezi kuwa baraka kweli kweli kwao wengine! Kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Kutoka sura ya 29, Mungu aliwaagiza makuhani watoe, “wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni …iwe harufu nzuri,… Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele…mbele ya Bwana. Hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo.” (29:38-42). Kumbe, Mungu Baba yetu anakutana nasi mahali pa madhabahu ya dhabihu naye anatazamia tutoe maisha yetu yawe harufu ya Yesu Kristo mbele Yake, ‘asubuhi na jioni’, yaani, wakati wote! (Yesu Kristo ni Mwana-Kondoo wa Mungu.) Na mahali pale pale pa sadaka anatutakasa ili tumtimikie tulipo. (“…nitaitakasa…hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.” 29:44). Jambo la ajabu! Kwa hiyo Paulo anasema, “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu aliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (War.12:1,2). Basi, usijisumbue kwa ajili ya mapenzi ya Mungu mawazoni mwako. Kwa kimsingi sasa unaijua njia. Njia ni Yesu Kristo. Lile usilolijua, subiri tu mbele Yake, na kwa wakati wake utalijua. Yatoe maisha yako yawe dhabihu iliyo hai, yawe harufu ya Kristo mbele Yake kila siku, bila kuitafuta njia yako mwenyewe, na neno la Mungu linatuambia utapata kujua hakika mapenzi ya Mungu, hatua kwa hatua na kwa wakati wake! Na kumbuka Paulo alilosema katika mstari unaofuata, yaani, “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunai.” Mungu akubariki!

na David stamen 2015

0 views0 comments

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page