Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
WATU wanane wamefariki dunia kutokana na mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa ya vifo hivyo Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema watu watano wametambuliwa na wengine watatu bado hawajatambulika na miili yao imehifadhiwa katika ya Hospitali ya Mwananyamala. Alisema Mei 6 mwaka huu, saa moja usiku maeneo ya Magomeni wilayani Kinondoni, mkazi wa Manzese, Shabani Idd (73), alisombwa na maji ya Mto Ng’ombe alipojaribu kuuvuka na mwili wake ulipatikana Mei 7 akiwa amefariki.
“Kifo kingine kilitokea Mei 7, mwaka huu mnamo saa 6 mchana maeneo ya Mwananyamala Mbuyuni ambako Masumbuko Douglass (50) alianguka na kufariki dunia ghafla wakati akitoa maji yaliyoingia ndani kwake na uchunguzi wa awali unaonyesha alikuwa na kifafa hivyo wakati akihangaika kutoa maji ugonjwa huo ulimpata na kuanguka,” alisema Kova. Alisema Mei 6, mwaka huu mkazi wa Mvuruhana Pemba Mnazi, Kigamboni, Rashidi Hassan (36), alizama katika mkondo wa maji unaoelekea baharini na mwili wake ulipatikana juzi ukiwa unaelea majini umbali wa mita 500 toka eneo alilozama. “Kifo kingine kimetokea Mei 6 mwaka huu eneo la Yombo Makangarawe ambako mtoto, Gloria Mrema mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu alipotea baada ya watoto wenzake kumuacha wakati wakicheza kwa pamoja na juhudi za kumtafuta zilifanyika bila mafanikio hadi mwili wake ulipopatikana ukiwa unaelea majini katika Mto Mzinga akiwa tayari amepoteza maisha na mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Temeke,” alisema Kova. Alisema kifo kingine kilitokea jana eneo la Kinondoni Mkwajuni baada ya mtu mmoja mwanaume jina lake halikufahamika anakadiriwa kuwa na umri kati miaka 40 au 45 alikutwa amefariki dunia na mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi. “Pamoja na vifo hivyo kuripotiwa, pia mtu mmoja Mabula Moses (65) ambaye ni mkazi wa Vingunguti wilayani Ilala amevunjika mguu wake wa kulia chini ya goti baada yakuangukiwa na ukuta wa ghala la Fida Hussen lililopakana na nyumba yake na majeruhi amepelekwa katika Hospitali ya Amana,” alisema Kova. Alisema katika Kata ya Mchikichini taarifa ya mafuriko inaonyesha nyumba takriban 70 zimefunikwa na maji hadi juu ya paa na wakazi wake tayari wamehama huku watu 35 wamejihifadhi Shule ya Sekondari Mchikichini. “Kata ya Jangwani zipo nyumba takriban 100 zimefunikwa na maji hadi juu ya paa na watu 300 walihama mapema. “Maeneo mengine yaliyoathirika zaidi kutokana na mvua hizo ni Keko, Changombe Maduka Mawili, Yombo Vituka, Vingunguti, Afrikana, Msasani Bonde la Mpunga, Jangwani, Manzese, Kigogo, Mburahati, Boko Basihaya na maeneo mengine taarifa hazijapokelewa,” alisema Kova. Aliwataka wananchi wote kuchukua tahadhari hasa wale wanaoishi maeneo ambayo ni mikondo ya maji au watumiaji wa barabara zinazopitiwa na mikondo hiyo.
MTANZANIA lilitembelea baadhi ya maeneo ya jiji hilo na kujionea hali halisi ya mafuriko na kukuta sehemu nyingi zikiwa zimezungukwa na maji. Pia mvua hizo zilisababisha zaidi ya kaya 80 katika kata za Wereweru, Masama, Rundugai na Mnadani wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kukosa makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.
Mbali na kaya hizo kukosa makazi, pia mafuriko hayo yameharibu vibaya miundombinu mbalimbali ya barabara ikiwemo madaraja kusombwa na maji pamoja na miundombinu ya reli kuharibika ikiwa ni pamoja na hekari 450 za mazao mbalimbali kuchukuliwa na maji.
Akizungumzia athari za mafuriko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Athony Mtaka, wakati akikabidhiwa msaada wa vifaa mbalimbali vya waathirika hao na Benki ya NMB, alisema mvua hizo zilizoanza kunyesha Mei 2, mwaka huu zilileta madhara makubwa kwa wananchi.
Kwa Mkoa wa Tanga, zaidi ya kaya 60 hazina mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Nyumba hizo zipo katika eneo la Magaoni, Donge na Mtaa wa Mabawa A zilizopo Kata ya Mabawa.
Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Mzamili Shemdoe, alithibitisha kupokea taarifa za kuwepo kwa kaya zilizoathirika na mvua hizo.
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema mvua hizo zitaendelea kwa muda wa siku 12 kuanzia leo. Habari hii imeandaliwa na Tunu Nassor, Esther Mnyika, Johanes Respichius na Herieth Faustine wa Dar es Salaam na Upendo Mosha wa Kilimanjaro na Amina Omari wa Tanga.
Global Radio Network
Comments