Vijana kutoka kaunti ya Nyamira chini ya mwavuli wa nationa youth council wamejitokeza kuwaunga wabunge wanne ambao walijitokeza jana na kulaumu utawala wa gavana wa kaunti ya Nyamira john Nyagarama kwa msingi wa ufisadi,ajira kwa njia ya ubaguzi na kutowapa vijana hitaji lao la kikatiba kufanya kazi ndani ya kaunti ya Nyamira. Akizungumza wakati wa kikao maalum na vijana wa kaunti ya Nyamira ndani ya mkahawa mmoja mjini Nyamira, mwakilishi wao katika kikao cha kitaifa patric makini Omweri alidai kuwa vijana wengi hawajaajiriwa kwa mujibu wa sheria huku idadi kubwa ya wazee wakionekana kuajiriwa kila kuchao. “Sio wote ambao tutapata ajira ndani ya kaunti ya Nyamira walakin gavana wa kaunti hajatenga nafasi za kazi kwa vijana jambo amabalo limepelekea vijana wa Nyamira kuwa wepesi wa kutumika na wendani wa gavana kuwasuta wote wanaompinga kwa hela kidogo”,alisema Makini. Aliendelea kusema kuwa kwa wakati mmoja kiongozi wa kundi lao alipoonyesha kupinga utawala wa kaunti jinsi unavyoshughulikia maswala ya vijana alighubikwa macho kwa ajira ambayo haikuwa ya kuwanufaisha vijana wa kaunti ya Nyamira. Kwa maendeleo kiongozi huyo alimtaka gavana wa kaunti kuweka wazi miradi ambayo amewekezwa na kaunti ilio na manufaa kwa wananchi hasa ukitoa mlinganisho wa kaunti zinazoizunguka kaunti ya Nyamira ilmradi wenyeji wawe na matumaini ya ufanisi wa maendeleo. Kiongozi wa Kitutu masaba kundi la nationa youth council Dominic Orori na katibu wao Speke Mainasso walitaka kundi la kupambana na ufisadi nchini kufanya uchunguzi kuhusu utumizi mbaya wa mamlaka kando na ufujaji wa hela uliokolea. Wote kwa pamoja waliapa kuitisha mkutano wa hadhara ndani ya kaunti ya Nyamira mwisho wa mwezi huu ili kuratibu maswala ambayo wanataka yafanyiwe mpangilio ulio wazi kulingana na uongozi wa kaunti ya Nyamira kwa msingi wa vijana. Haya yamejiri siku moja tu baada ya wabunge wanne,james Geni-north mugirango,Timothy Bosire-kitutu masaba,James Gesami west mugirango na mwakilishi wa kina mama Alice Chae kutoka kaunti ya Nyamira kuandaa kikao na waandishi wa habari kuelezea ghathabu yao kuhusu kile kulingana nao ni utawala mbaya,ufisadi na ubaguzi katika miradi ya ajira na maendeleo.
top of page
bottom of page
Comments